Ukadiriaji na Maoni kwenye Duka la Google Play
Kwenye ukurasa huu unaweza kupata maelezo kuhusu ukadiriaji na maoni kwenye Google Play, pamoja na sera za Google za kuchapisha maoni.
Unaweza kuandika maoni kuhusu kitu chochote ambacho umenunua au kukodisha kutoka Google Play. Maoni ni njia nzuri sana ya kuwasaidia wengine kuamua cha kununua kwa kuwaambia kuhusu hali yako ya utumiaji. Google haimlipi mtu yeyote kukadiria au kuandika maoni kuhusu maudhui kwenye Google Play na tunatarajia wanaotoa maoni wawe waaminifu na wasipendelee upande wowote.
Jinsi ukadiriaji hukokotolewa
Ukadiriaji wa programu kwenye Duka la Google Play na grafu za pau zinazolingana ambazo zinaonyesha uwiano wa maoni ya nyota 1, 2, 3, 4 na 5, hukokotolewa kulingana na ukadiriaji wa sasa wa ubora wa programu kutoka kwa maoni ya mtumiaji, badala ya thamani ya wastani ya maoni ya watumiaji ya siku zote, isipokuwa kama programu ina makadirio machache sana. Kwa vile programu zinaweza kubadilika kadiri muda unavyosonga na vipengele vinaongezwa na kuondolewa mara kwa mara, hatua hii huwapa watumiaji maarifa zaidi kuhusu programu na ufahamu bora wa hali yake ya sasa. Tunaonyesha idadi ya jumla ya maoni ya siku zote kwa kuwa hii huwapa watumiaji taarifa muhimu kuhusu matumizi na muda wa matumizi ya programu.
Ukadiriaji wa maudhui mengine kwenye Duka la Google Play (vitabu, filamu, vipindi vya televisheni) hukokotolewa kulingana na thamani ya wastani ya maoni ya siku zote ya watumiaji wa maudhui hayo.
Kile ambacho wengine wataona unapoandika maoni
Maoni mengi huonekana kwa kila mtu na programu ya Duka la Google Play itaonyesha iwapo maoni yako yataonekana kwa umma au ni ya faragha.
Katika maoni yanayoonekana kwa umma, yeyote anayetumia Google Play (ikiwa ni pamoja na wasanidi programu) ataona jina na picha kutoka kwenye Akaunti yako ya Google, pamoja na mabadiliko ya awali uliyofanya kwenye maoni wako. Maoni ya faragha kwa kawaida hutolewa kuhusu programu zilizo katika toleo la Beta au jaribio la beta. Katika hali hii, maoni yako, ikijumuisha jina na picha kutoka kwenye Akaunti yako ya Google, pamoja na mabadiliko ya awali uliyofanya kwenye maoni yako, yataonekana kwa msanidi programu pekee. Katika ukaguzi wa umma na wa faragha, wasanidi programu wanaweza pia kuona maelezo ya lugha, kifaa, nchi uliko pamoja na maelezo ya kifaa (kama vile lugha, muundo na toleo la OS). Wasanidi programu pia wanaweza kujibu maoni na wanaweza kutumia maelezo haya kukujibu. Ukibadilisha maoni, watumiaji wengine na wasanidi programu bado wanaweza kuona mabadiliko ya awali isipokuwa ufute maoni hayo.
Sera za kuchapisha ukadiriaji na maoni
Ukadiriaji na maoni yanapaswa kuwa ya kuaminika na yanayosaidia. Kutoa maoni kuhusu maudhui kwenye Google Play ni njia nzuri ya kushiriki maoni muhimu na kuwasaidia watumiaji wengine wa Google Play kupata maudhui na huduma bora.
Mwongozo wa jinsi ya kuandika maoni mazuri
- Yafanye maoni yako yawe ya manufaa na yanayoelimisha.
- Jaribu kujumuisha hali zote mbili, mambo mazuri na changamoto
- Yafanye yawe rahisi kusomeka; kagua sarufi na tahajia na usitumie herufi kubwa na alama za uakifishaji kupita kiasi.
- Waheshimu wengine.
Sera za Google Play za ukadiriaji na maoni ziko hapa chini. Maoni ambayo yanakera au yanakiuka sera hizi yataondolewa kupitia mchanganyiko wa uhakiki wa kiotomatiki na unaofanywa na binadamu na yeyote anayekiuka sera hizi mara kwa mara au anayekiuka kwa kupitiliza, anaweza kupoteza uwezo wa kuchapisha kwenye Duka la Google Play.
Taka na maoni bandia
Maoni yako yanapaswa kuonyesha hali yako ya utumiaji wa maudhui au huduma unayotolea maoni.
- Usichapishe maoni bandia au yasiyo sahihi.
- Usichapishe maoni yale yale mara nyingi.
- Usichapishe maoni kuhusu bidhaa sawa ukitumia akaunti nyingi.
- Usichapishe maoni ili kuwapotosha watumiaji wengine au kubadilisha ukadiriaji.
- Usichapishe maoni kwa niaba ya wengine.
- Usiwakilishe kwa uongo utambulisho au uhusiano wako na maudhui unayotolea maoni.
Maoni yaliyo nje ya mada
Andika maoni yanayolingana na mada na yanayohusiana na maudhui, huduma au hali ya utumiaji unayotolea maoni.
- Usichapishe uombaji, maoni ya kisiasa au kijamii au chochote kisichohusiana na maudhui, huduma au hali muhimu ya utumiaji ya mteja unayotolea maoni.
Utangazaji
Tunataka maoni yawe ya kufaa na hayatakuwa ya kufaa ikiwa yanatangaza kitu kingine tofauti na maudhui au huduma unayotolea maoni.
- Usichapishe maudhui ya matangazo au ya biashara ya bidhaa au huduma zozote, ikiwa ni pamoja na matangazo ya washirika au ya kuelekeza wateja.
- Usichapishe nambari za simu, anwani za barua pepe au viungo vinavyoelekeza kwenye tovuti nyingine.
Mgongano wa maslahi
Maoni ni muhimu zaidi yakiwa ya kweli na yasiyopendelea upande wowote. Yanapaswa kuandikwa na watu wasio na nia ya kunufaika kifedha.
- Usitoe wala kukubali pesa, bidhaa au huduma kama malipo ili kuchapisha maoni.
- Usitoe maoni kuhusu maudhui, huduma au hali ya utumiaji ikiwa unamiliki au unafanyia kazi biashara iliyoitayarisha.
Maudhui yaliyo na hakimiliki
Maoni yanapaswa kuwa yako mwenyewe na yaonyeshe mawazo yako binafsi.
- Usichapishe maoni yanayokiuka haki za uvumbuzi za wengine ikiwemo hakimiliki.
Pata maelezo kuhusu jinsi ya kuondoa maudhui yaliyo na hakimiliki
Maelezo ya kibinafsi na ya siri
Maoni yanalenga kushiriki hali ya utumiaji na unaweza kueleza hisia yako kuhusu kitu fulani bila kufichua taarifa nyeti za kibinafsi.
- Usichapishe taarifa binafsi au ya siri kama vile anwani ya mahali halisi au nambari ya leseni ya udereva.
Maudhui yanayokiuka sheria
Ni sharti maoni yako yatii sheria na masharti au makubaliano yoyote ya kisheria ambayo umekubali.
- Usichapishe maoni yaliyo na au yanayoelekeza kwenye maudhui yasiyo halali.
Maudhui dhahiri ya ngono
Google Play inalenga hadhira pana na maoni yanapaswa kuonyesha hilo.
- Usichapishe maoni yaliyo na, yanayokuza au kuomba maudhui dhahiri ya ngono.
- Usichapishe maoni ambayo yanaonyesha watoto katika hali za kingono au kuwazungumzia kwa namna ya kingono.
Matamshi ya chuki
Google Play inalenga watu wote na maoni yanapaswa kuonyesha hilo.
- Usitangaze vurugu, kuunga mkono vurugu au kuchochea chuki dhidi ya mtu binafsi au kikundi cha watu kwa misingi ya mbari, uraia, kabila, dini, jinsia, utambulisho wa kijinsia, mwelekeo wa kingono, umri, ulemavu, hali ya kuwahi kuwa mwanajeshi mstaafu au sifa zingine zozote zinazohusiana na ubaguzi au ubaguzi wa kimfumo.
Maoni ya kukera
Google Play inalenga kuburudisha na kuwapa watu taarifa wala si kuwashambulia na kuwakera.
- Usichapishe lugha yenye matusi, lugha chafu au lugha ya kukera.
- Usichapishe maoni yanayonyanyasa, kuwachokoza au yanawashambulia wengine.